0
Kanuni ya kumjua Mungu ipo hivi:

Hauwezi kuja kwa Yesu bila kuitwa na YEHOVA ~ (YOHANA 6:44;65); hauwezi kumjua Roho Mtakatifu bila kufundishwa na Yesu ~ (YOHANA 15:26); hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu bila kupewa na Yesu ~ (YOHANA 20:22); na hauwezi kwenda kwa YEHOVA bila kuongozwa na Yesu ~ (YOHANA 14:6).

Zingatia kwamba; Pasipo Yesu hauwezi kufanya lolote ~ (YOHANA 15:5); na pia kila mtu asiye na Roho Mtakatifu ndani yake huyo si mwanafunzi wa Yesu. ~ (WARUMI 8:9).

Ni lazima kwanza KUITWA NA YEHOVA, pili KUMPOKEA YESU, na ndipo utakapompata Roho Mtakatifu; Naye Roho Mtakatifu akaapo ndani yako daima ndipo unapata uzima wa milele. 

Inawezekana ukawa jambo hili usilielewa hata ukajiuliza;
 



NINI MAANA YA KUFUNDISHWA NA YESU? Au NITAWEZAJE KUFUNDISHWA NA YESU?



Maana ya kufundishwa na Yesu ni hivi; Tunaposoma Injili ya Mathayo sura ya 28 tunaona Bwana Yesu anawaambia wanafunzi Wake kwamba:
"...enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi... na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi..." ~ 
MATHAYO 28:19-20.Hapo Yesu alikuwa anaongea ana kwa ana na wale wanafunzi ambao walimwona na waliyapokea mafundisho Yake moja kwa moja; lakini tunaona anawaambia waende kufanya mataifa (watu wasiomjua Yeye) ili wawe wanafunzi kwa kuwafundisha kuyashika YOTE ambayo Yesu amawapa amri kuyafanya. Si kwamba kila mmoja wao akafundishe jinsi atakavyo yeye, bali anafundisha kile alichoamriwa na Yesu. Kwa hiyo kwa maana nyepesi ni kwamba Yesu anasema nasi kupitia watu hao.
Hebu chukulia mfano huu mwepesi: Mf. Rais akimpa ujumbe Waziri akahutubie taifa, na Waziri huyo akahutubia kile tu alichoambiwa na Rais pasipo kuongeza neno wala kupunguza neno; je! Hapo si nisawa na Rais kazungumza na taifa kupitia Waziri? Japokuwa anayeongea ni Waziri lakini anasema ujumbe kutoka kwa Rais. Vivyo hivyo nasi tunafundishwa na Yesu kupitia vinywa vya watumishi Wake. Kuna jambo hili zuri najifunza kwa Mtume Paulo, anasema kwamba:
"Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akisema, Huu ndio mwili Wangu ulio kwa ajili yenu..." ~ 1 WAKORINTHO 11:23-24.
Hapo Mtume Paulo anasema: "...mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi..." Umewahi kujiuliza swali hili;



Je! Mtume Paulo alikuwepo siku ile ambayo Yesu anaumega mkate? Kama hakuwepo; Inakuwaje aseme: "...mimi nalipokea kwa Bwana..."?



Mtume Paulo amepata ujasiri wa kusema “MIMI NALIPOKEA” kwa sababu yeye Paulo alifundishwa na Yesu kupitia watumishi wa Yesu; vivyo hivyo na sisi tu watumishi wa Yesu ambao Yesu Mwenyewe anasema nasi kupitia neno lile ambalo ametuagiza kulisema. Hivyo basi; ninaposema kuwa hauwezi kumjua Roho Mtakatifu bila kufundishwa na Yesu; hapo ninamaanisha kwamba: Yesu Kristo ndiye ametufunulia namna ya kumjua Mungu. Haiwezekani mtu akamkubali Roho Mtakatifu bila ya kwanza kuyakubali mafundisho ya Yesu, kwa maana wote wasiomkubali Yesu kamwe hawawezi kuukubali Utatu Mtakatifu wa Mungu. Bwana Yesu anasema:
...maana pasipo Mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote." ~ YOHANA 15:5.
Pasipo Yesu haiwezekani kumjua Mungu, na wala haiwezekani kumshinda Shetani. Bwana Yesu ndiye atupaye akili ya kumjua Mungu pamoja na kutufanya sisi kuwa watu wa milki ya Mungu. Kuwa milki ya Mungu maana yake ni kwamba sisi ni mali ya Mungu kwa sababu Mungu yupo nasi na anakaa ndani yetu.

Bwana Yesu anasema kwamba:

"Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu." ~ YOHANA 14:16-17.
Yesu anasema: "... ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui..."
Ulimwengu haumtambui ni kwa sababu ulimwengu umemkataa Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wao. Ukimkataa Yesu maana yake ni kuyakataa mafundisho Yake; na mtu akiyakataa mafundisho YOTE ya Yesu maana yake mtu huyo anakuwa gizani kwa sababu ameikataa nuru. Ndio maana ulimwengu HAUMTAMBUI Roho Mtakatifu.
Pia Yesu anasema kwamba ulimwengu HAUMWONI Roho Mtakatifu kwa sababu Yeye hakai ndani yao. Kama Roho Mtakatifu hayumo ndani yako kamwe hauwezi kuuona utendaji Wake akikutumia katika maisha yako. Roho Mtakatifu ni Mungu atupatiaye NGUVU za kushinda vita vyote vya mwilini na rohoni. Kwa hiyo ulimwengu hauwezi kumpokea Roho Mtakatifu kwa sababu wenyewe umemkataa Yesu ambaye ndiye atuongozaye kumjua Mungu.
 

Post a Comment

Emoticon
:) :)) ;(( :-) =)) ;( ;-( :d :-d @-) :p :o :>) (o) [-( :-? (p) :-s (m) 8-) :-t :-b b-( :-# =p~ $-) (b) (f) x-) (k) (h) (c) cheer
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.

 
Top